Wednesday, October 5, 2011

Rais Kikwete akagua bwawa la kuzalisha umeme Kidatu

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikagua mitambo ya kuzalisha umeme katika bwawa la Kidatu,mkoani Morogoro jana .Kushoto ni meneja wa TANESCO wa mkoa na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumatano, Oktoba 5, 2011, ametembelea bwawa la uzalishaji umeme wa gridi ya taifa la Kidatu, mkoani Morogoro kujionea mwenyewe kina cha maji katika bwawa hilo, moja ya vianzio vikubwa vya umeme nchini.
Rais Kikwete amesimama na kuangalia bwawa hilo kwa muda mfupi tu baada ya kuwa amefunga mafunzo ya uchunguzi na upelelezi wa maofisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kwenye Chuo cha Polisi kilichoko hapo hapo Kidatu.
Kwenye bwawa hilo, Mheshimiwa Rais ameambiwa na Kaimu Meneja wa Uzalishaji Umeme Kidatu, Mhandisi Joseph Lyaruu kuwa hali ya uzalishaji umeme kutoka Kidatu bado ni mbaya kwa sababu ni megawati 40 tu za umeme zinazozalishwa kwenye bwawa hilo kwa sasa kulinganisha na uwezo wa uzalishaji wa megawati 200 kwa sababu ya kupungua kwa kina cha maji kwenye bwawa hilo.
Mhandisi Lyaruu pia amemweleza Mheshimiwa Rais Kikwete kuwa hata uzalishaji umeme katika bwawa jingine la Mtera lililoko mkoani Iringa bado ni mdogo sana kwa sababu bwawa hilo linazalisha kiasi cha megawati 30 tu kati ya megawati 80 zinazoweza kuzalishwa kwenye bwawa hilo kama yapo maji ya kutosha.
“Hali bado mbaya,” Mheshimiwa Rais amesema baada ya kuwa ameelezwa na Mhandisi Lyaruu kuhusu hali hiyo ambayo imesababisha mgawo mkubwa wa umeme nchini kwa miezi kadhaa sasa na kupelekea Serikali kuchukua hatua za dharura za kuzalisha umeme kutokana na vyanzo vingine.
Akiwa njiani kuelekea Ifakara kutoka Kidatu, Mheshimiwa Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku tatu ya Mkoa wa Mogororo amesimama kwa muda katika Kijiji cha Mkula kupata maelezo kuhusu skimu ya umwagiliaji ya kilimo cha mpunga, ambayo aliifungua mwaka 2008 wakati wa ziara nyingine ya mkoa huo.
Kwenye kijiji hicho, Rais Kikwete ameambia kuwa kutokana na skimu hiyo ya umwagiliaji ambayo ilijengwa kwa kiasi cha sh milioni 276 za Serikali, wananchi wa kijiji hicho sasa wameongeza uzalishaji wa mpunga hadi kufikia tani 7.6 kwa ekari moja kutoka tani 1.5 iliyokuwa inavunwa kabla ya kuanza umwagiliaji.
Wanakijiji hao wamemwambia Mheshimiwa Rais: “Tumesikia unapita na tukaamua kujikusanya kukushukuru kwa msaada wako. Uliahidi kutupatia power tillers tano na tayari tumekwishakupokea nne. Tulikuwa tunalina ekari 12 tu kabla ya skimu ya umwagiliaji kujengwa na sasa tunalipa ekari 100 kati ya eneo la ekari 254 za eneo hili. Tunakushukuru sana kwa sababu yote uliyotuahidi ulipofika hapa mwaka 2008 yametimizwa.”
Wameongeza wanakijiji katika risala yao: “Kipato chetu kimeongezeka kiasi cha kutosha Mheshimiwa. Tunacho chakula cha kutosha na ziada kubwa ya kuuza. Tunaweza sasa kulipa ada ya wanafunzi wa shule yetu, tuna chakula mwaka mzima, tunazo pesa za matibabu na tuna uwezo wa kuchangia miradi mbali mbali ya maendeleo.”
Wasema wana-kijiji hao: “Ni viongozi wachache sana wanaoahidi kuwatembelea tena wanavijiji na wakafanya hivyo, tena kututembelea sisi kwenye hii vumbi. Kama ungekuwa mchezaji wa mpira hakuna shaka kuwa ungenunuliwa kwa bei mbaya.”
Mheshimiwa Rais leo amelala mjini Ifaraka na kesho ataendelea na ziara yake mkoani Morogoro ikiwa ni siku ya tatu na ya mwisho ya ziara hiyo.

No comments: