MTAFARUKU mkubwa umeibuka wa kugombea maiti na mali zake, kati ya ndugu wa marehemu, mumewe na mwajiri. Dada wa marehemu anadai kadi za benki huku mwajiri naye akitaka vyombo vya ndani kwa madai kuwa fedha alizovinunulia alikopa kazini. Rahima Hamad (24) alifariki dunia Machi 4 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro baada ya kujifungua mtoto njiti, hospitalini hapo. Akizungumza na gazeti hili jana, mume wa marehemu, Matheo Juma, alidai kuwa yeye na mkewe (marehemu), waliishi kwa miaka sita, lakini cha kusikitisha ni kwamba upande wa familia ya marehemu wamekana kumtambua. Alidai kwamba awali ndugu wa mkewe walikuwa wakifika nyumbani kwake na kupata huduma mbalimbali, lakini baada ya kifo hicho wamemkana na kudai kuwa marehemu hakuwa na mume, hivyo mazishi hayawezi kufanyika sehemu nyingine tofauti na alikozaliwa kijijini kwao Rombo. Juma alidai kuwa awali mkewe alikuwa Mkristo, na kubadilisha dini kwa ridhaa yake kuwa Mwislamu, na kisha kutambulishwa kwa wazazi wa mke kwa ajili ya mchakato wa kufunga ndoa naye. Alisema mara baada ya msiba huo kutokea kaka wa marehemu, Doe Swai, alimkana na akidai kuwa dada yao hakuwa na mume, huku akimtuhumu yeye kuhusika na kifo hicho kutokana na ujauzito, hivyo maiti lazima azikwe kwa misingi ya kikristo. Juma aliendelea kudai kwamba mbali na hilo, pia dada wa marehemu aliyetambuliwa kwa jina la Eliza na mwajiri wa marehemu, Stella Sembeti, wanadai mali zilizoachwa na marehemu vikiwamo vyombo vya ndani, kadi za benki na nguo wakati huu ambao hata maziko hayajafanyika. Alidai kwamba kutokana na hali hiyo, ametishiwa maisha endapo atahudhuria mazishi na kama ataendelea kung’ang’ania mwili wa marehemu. Kwa upande wao, majirani wa marehemu walisema wakati mwajiri na dada wa marehemu walipofika kudai mali hizo, wananchi walijikusanya kwa lengo la kuwapiga lakini fujo hizo zilitulizwa na Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa na kuamuru vyombo hivyo vihamishwe ili viwekwe sehemu yenye usalama kwa usimamizi wake. Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Eliza alikiri kuwapo mvutano huo, na kueleza kuwa hawezi kumtambua mwanamume aliyekuwa akiishi na dadake kwani hana cheti cha ndoa, na mila za Wachaga haziruhusu azikwe nje ya familia. Eliza alisema uamuzi wa kumzika marehemu nyumbani kwa wazazi wake unazingatia wosia alioandika marehemu na kuwaeleza watoto wake kuwa akifariki dunia azikwe kwa baba na mama yake. Alisema mbali na hayo, hawezi kumtambua kwa sababu hajawahi kutoa mahari, hivyo hana uhalali na mwili wa marehemu, huku akidai kuwa mali zote ni za marehemu kwa kuwa mume huyo hakuwa na kitu chochote tangu walipoanza kuishi. Eliza alieleza kuwa mdogo wake awali aliolewa na mume mwingine kwa ndoa ya Kanisa Katoliki, hivyo anayedai kuwa mumewe wa sasa alimnyang’anya mume mwingine, hivyo akahamishia mali zote kwake. Akizungumzia mali anazozidai, Eliza alisema mali zote ni za dada yao, na kuwa kadi ya benki marehemu aliihamishia kusikojulikana; na wakati mazungumzo na gazeti hili yakiendelea Eliza alinyang’anywa simu na mwanamume ambaye alidai, “hapa tupo kwenye msiba,” na kukata simu na kuizima. Gazeti hili pia lilimpata aliyekuwa mwajiri wa marehemu –Sembeti, ambaye alikiri Rahima (marehemu) alikuwa mfanyakazi wake katika hoteli ya Kiusa Pub akiwa Meneja mjini hapa. Akizungumzia madai ya kutaka mali za ndani za Rahima, alisema ni kweli alimkopesha Sh 130,000 kwa ajili ya kununulia godoro, lakini alikanusha kudai godoro hilo au fedha.
No comments:
Post a Comment